Habari

BARAZA LA USHINDANI LATOA ELIMU YA UWASILISHAJI WA RUFAA KUPITIA MFUMO WA KIDIJITALI
  • 21 Dec, 2025
BARAZA LA USHINDANI LATOA ELIMU YA UWASILISHAJI WA RUFAA KUPITIA MFUMO WA KIDIJITALI

Baraza la Ushindani (FCT) limeendesha Semina ya Elimu kwa Wadau iliyofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mbeya, yenye lengo la kuwajengea wadau uelewa kuhusu majukumu, huduma na mifumo ya kisasa inayotumiwa na Baraza hilo katika utoaji wa haki.

 

Mgeni rasmi katika semina hiyo alikuwa Bi. Anna Mwambene, Katibu Tawala Msaidizi – Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mkoa wa Mbeya, ambaye alifungua semina hiyo kwa kuhimiza wadau kushiriki kikamilifu katika mafunzo na kuwa mabalozi wa kuitangaza huduma za Baraza la Ushindani (FCT) kwa jamii.

Katika hotuba yake, Bi. Mwambene alisisitiza umuhimu wa elimu ya ushindani katika kukuza mazingira bora ya biashara na uwekezaji, akieleza kuwa uelewa wa sheria na taratibu za rufaa husaidia kulinda haki za wafanyabiashara na kuimarisha uchumi wa taifa.

 

Kupitia semina hiyo, Baraza la Ushindani limewapatia washiriki mafunzo kuhusu namna linavyotoa huduma zake, hususan matumizi ya mfumo wa kidijitali wa kuwasilisha rufaa zinazotokana na maamuzi ya Tume ya Ushindani (FCC) pamoja na mamlaka za udhibiti ambazo ni LATRA, EWURA, TCRA, TCAA na PURA.

 

Akitoa mada kuhusu matumizi ya mfumo huo, Afisa TEHAMA wa Baraza la Ushindani, Bw. Athumani Kanyegezi, aliwaelezea wadau hatua kwa hatua jinsi ya kuutumia mfumo wa kidijitali wa uwasilishaji wa rufaa.

“Kwa njia ya mtandao, mtu anaweza kuanzisha akaunti, kujaza fomu ya rufaa, kupakia nyaraka muhimu, kulipa ada na kufuatilia mwenendo wa kesi yake ndani ya mfumo bila kuhitaji kutembelea ofisi zetu,” alisema Bw. Kanyegezi.

 

Semina hiyo ilihusisha wafanyabiashara, wajasiriamali pamoja na wawakilishi wa taasisi mbalimbali, ambapo washiriki walipata fursa ya kuuliza maswali na kupata ufafanuzi kuhusu taratibu za rufaa, matumizi ya mfumo wa kidijitali na umuhimu wake katika kurahisisha upatikanaji wa haki kwa wakati.

 

Baraza la Ushindani (FCT) limeeleza kuwa litaendelea kutoa elimu kwa wadau katika mikoa mbalimbali nchini ili kuongeza uelewa wa jamii kuhusu ushindani wa haki na matumizi sahihi ya mifumo ya kisheria iliyopo.