Habari
FCT YAWEZESHA WADAU MOSHI, MAHITAJI YA ELIMU YAVUTA WENGI
- 24 Jan, 2026
MOSHI: Baraza la Ushindani (FCT) jana tarehe 21 Januari, 2026, limeendesha mafunzo ya uwezeshaji kwa wadau mbalimbali jijini Moshi, mkoani Kilimanjaro, yaliyojumuisha wafanyabiashara na wananchi, kwa lengo la kuwajengea uelewa kuhusu masuala ya ushindani, haki za kibiashara na mifumo ya kisasa ya utoaji wa haki. Mafunzo hayo yalishuhudia mwitikio mkubwa wa wadau, hali iliyoonesha mahitaji makubwa ya elimu kuhusu taratibu za kisheria na huduma zinazotolewa na Baraza la Ushindani.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Msajili wa Baraza la Ushindani, Mhe. Mbegu Kaskasi, aliwashukuru wadau wa Moshi kwa kujitokeza kwa wingi na kuonesha hamasa ya kujifunza, akieleza kuwa hilo ni chachu ya kuimarisha mazingira ya biashara yenye ushindani wa haki. Mhe. Kaskasi alieleza kuwa Baraza la Ushindani linaendelea kuboresha mifumo yake ili kurahisisha upatikanaji wa haki, ikiwemo mfumo wa kielektroniki wa uwasilishaji wa mashauri ya rufaa, ambao umepunguza gharama na usumbufu wa kusafiri kwa wadau waliokuwa wakilazimika kufika moja kwa moja katika ofisi za Baraza.
Ameongeza kuwa mfumo huo umeimarisha pia usalama wa taarifa za wadau na kurahisisha uhifadhi na upatikanaji wa kumbukumbu kwa wakati, hatua inayochangia kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma. Baadhi ya wadau walioshiriki mafunzo hayo walieleza kunufaika kwa kiasi kikubwa na elimu waliyoipata, wakisema imewasaidia kuelewa haki zao, wajibu wao na taratibu za kufuata wanapohitaji kuwasilisha mashauri yao. Mhe. Mbegu Kaskasi amesisitiza kuwa FCT itaendelea kutoa elimu kwa wadau katika mikoa mbalimbali nchini, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu yake na kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita ya kuimarisha mazingira ya biashara na kulinda ushindani wa haki nchini.

